Na Elinipa Lupembe
Waziri wa Utalii na Malikale Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga, ametangaza rasmi kufanyika kwa maonesho ya Kimataifa ya Utalii Visiwani Zanzibar kuanzia Oktoba 25- 26, 2024 huku akiwaalika wadau wote wa utalii kushiriki kwenye maonesho hayo makubwa na ya kihistoria.
Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga amezungumza, wakati akizindua rasmi msimu wa maonesho hayo yatakayokwenda kwa jina la Zanzibar Tourism and Investment Show 2024, uliofanyika kwenye banda la Kamisheni ya Utalii Zanzibar, kwenye viwanja vya Magereza Kisongo Mjini Arusha mapema leo Juni 08, 2024, ikiwa ni siku ya pili ya Maonesho ya Karibu Kili Fair 2024 mkoani Arusha.
Mhe. Mudrick amesema kuwa, maonesho hayo yanatarajiwa kutambulisha fursa mbalimbali za kiutalii na uwekezaji zilizopo kwenye sekta ya utalii Zanzibar pamoja na nafuu za Serikali katika uwekezaji, zoezi ambalo litafanyika kwenye viwanja vya Dimani mwezi Oktoba 2024.
"Kufanyika kwa maonesho hayo ni muendelezo wa kuutangaza utalii na fursa zilizopo kwenye utalii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuchagiza na kuchochea tija ya kiuchumi na kijamii inayotokana na sekta ya utalii, katika kuunga jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais Dkt. Hussein Mwinyi wa Zanzibar" Amefafanua Mhe.
Hata hivyo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni washiriki wa maonesho ya Karibu - Kili Fair 2024 ambapo wakati wa Uzinduzi wa maonesho haya, Waziri Mudrick alitaka kubuniwa kwa mkakati wa kimawasiliano ili kufanikisha ombi la Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda la kutaka Zanzibar na Arusha kuungana katika kukuza utalii.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.